Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi, amefanya ibada na kusema: “Namshukuru Mungu kwa kumponya.”
Ni mara ya kwanza Saro kuzungumza tukio hilo tangu aliporuhusiwa kutoka Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu, MOI ya Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa.Hakika @Ufoo Saro aliokoka kuuliwa mwaka jana mwishoni@
Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba, Jimbo la Magharibi, Ufoo huku akitokwa na machozi na wakati mwingine kushindwa kuzungumza alisema: “Ni miujiza tu ya Mungu yeye kunifanya mimi kuwa hai leo.”
Mtangazaji huyo ambaye alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili, aliwashukuru watu wote waliomtia moyo, kumsaidia kipindi chote alichokuwa mgonjwa.
“Sina cha kuwalipa, ninawashukuru sana kwa wema wenu, pia kwa kuniombea. Mungu ni mkubwa na amenipigania, naendelea vizuri kwa sasa,” alisema na kuongeza:
“Mungu alinisimamia na nyinyi pia mliniombea, hakika sina budi kushukuru kwa kila jambo. Nitasoma zaburi ya 146 katika Biblia Takatifu ili kumshukuru Mungu kwa kunisaidia.”
Ufoo alisema kuwa ameamua kumshukuru Mungu kwa sababu siyo watu wote wanaopata matatizo kama yake wanapona.
Mchungaji aliyeongoza misa hiyo iliyoanza saa 1 asubuhi hadi saa 5 asubuhi,Joseph Maseghe alisema Mungu hakupanga Ufoo afariki dunia kwa kupigwa risasi.
“Mungu bado anakuhitaji, hakupanga ndiyo maana upo nasi leo. Hautakiwi kulia huu ni mwanzo wa maisha yako mengine, usilie unachotakiwa ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema.